Juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kupiga marufuku unywaji na uuzwaji wa pombe hasa zile zilizofungwa kwenye mifuko aina ya viroba ziambatane na uundwaji wa sera ya pombe ya Taifa itakayosaidia katika kudhibiti matumizi ya vilevi hapa nchini.
Sera ya hiyo italazimisha sheria zinazoambatana kurekebishwa ambapo pia zitawawezesha wafanyabiashara, watengenezaji na wauzaji wa kinywaji hicho kutambua haki, madhara na makosa yao mapema katika utoaji huduma, na hiyo itaisaidia serikali katika usimamizi madhubuti, na mwenendo wa udhibiti utakuwa wazi tofauti na sasa ambapo serikali imeamua kupiga marufuku kwa kushtukiza, jambo ambalo limepelekea kuleta madhara kwa wafanyabiashara ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa wanajua madhara yake.
Matumizi ya pombe aina ya viroba hayana budi kuwekewa sera, na sheria ziboreshwe hasa juu ya matumizi kwani yanachangia madhara makubwa ya kiafya kwa jamii pamoja na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, migogoro majumbani, utelekezaji wa familia, ubakaji, ajali barabarani na pengine kuharibu nguvu kazi ya jamii na taifa kwa ujumla
Chama cha Wanahabari Wanawake – TAMWA, kupitia kupitia kituo chake cha usuluhishi (CRC), kimekuwa kikiomba uwepo wa sera ya Taifa juu ya matumizi ya Pombe nchini kama ilivyo nchini Kenya na Uganda, aidha kimekuwa kikitoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya pombe kupita kiasi ambapo kwa mwaka 2016 kiliweza kuwapa ushauri nasihi wananchi wapatao 490, kati ya hao wanawake walikuwa 355, wanaume 92 na watoto walikuwa 45 walioathirika kwa namna mbalimbali kutokana na unywaji pombe kupindukia.
Edda Sanga
Mkurugenzi Mtendaji
↧