Chama cha Wanahabari Wanawake nchini kinaungana na mashirika ya kihabari nchini kote kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ulimwenguni ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 3 Mei ambapo mwaka huu kitaifa yatafanyika mjini Mwanza.
Maadhimisho hayo ambayo kauli mbiu yake mwaka huu ni “Fikra Yakinifu kwa wakati Muhimu; Jukumu la Vyombo vya Habari katika kuendeleza Jamii zenye Amani, Haki Jumuishi” TAMWA imewataka wanahabari kote nchini kufanya kazi zao kwa weledi hasa katika kuhakikisha wanazingatia usawa katika kutoa taarifa mbalimbali zikiwemo zile zinazohusu wanawake,watoto na wanaume.
Aidha katika maadhimisho ya mwaka huu, TAMWA inawapongeza wanahabari na vyombo vya habari nchini kwa jinsi vinavyoshirikiana katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatolewa taarifa bila woga na wahusika wanachukuliwa hatua stahiki kwakua vitendo hivyo huchangia katika kurudisha nyuma maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.
TAMWA katika mpango mkakati wake wa kuelimisha jamii kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto, kwa kipindi cha mwaka 2015 na 2016 wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini zaidi ya wanahabari 2,350 na wahariri 120 walijengewa uwezo wa jinsi ya kuandika habari za ukatili wa kijinsia zenye kuleta mabadiliko katika jamii ambapo kwa sasa vitendo hivyo vinatolewa taarifa kwa usahihi ukilinganisha na awali.
TAMWA katika kutekeleza mradi wake wa GEWE II kimeweza kuhunda kamati za kuelimisha jamii jinsi ya kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya kumi za Tanzania na Bara na visiwani ambazo zinawahusisha wanahabari ili kuziwezesha jamii kushirikiana na vyombo vya habari kuweza kuvitolea taarifa vitendo hivyo bila woga ambapo kamati hizo zimesaidia kuibua matukio hayo.
TAMWA inaamini kuwa kupitia maadhimisho haya wanahabari kote nchini watafanya kazi zao kwa weledi na uaminifu na kuandaa habari zenye usawa wa pande zote husika pamoja na kuibua mambo yanayoweza kukwamisha jitihada za maendeleo ili yafanyiwe kazi pia kujihepusha na habari ambazo kwa sehemu zinaweza kuleta machafuko na kuhatarisha maisha yao wenyewe au wananchi katika taifa la Tanzania.
Edda Sanga
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA
↧