Quantcast
Channel: TAMWA - TAMWA - PRESS RELEASE
Viewing all articles
Browse latest Browse all 40

MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA UNAOTETEA MAREKEBISHO YA SHERIA NA SERA INAYOHUSU USALAMA BARABARANI TANZANIA

$
0
0
Mapendekezo ya Maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani kwa mtazamo wa visababishi vitano vya ajali Mtandao wa wadau kutoka Asasi za Kiraia unaotetea Marekebisho ya Sheria na Sera inayohusu Usalama Barabarani Tanzania, umeungana na watanzania katika Maadhimisho ya Nne ya Umoja wa Mataifa ya Wiki ya Usalama Barabarani (UN Road Safety Week) yalionza tarehe 08/05/2017 na kufikia kilele chake tarehe 14/05/2017. Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni “Udhibiti wa Mwendo Kasi kwa Vyombo vya Usafiri”. Wakati tunaadhimisha Wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani, tumeshuhudia matukio mbalimbali ya ajali ambazo chanzo chake kikubwa ni makosa ya kibinadamu. Mfano mmojawapo ni ule wa tukio la tarehe 6 Mei mwaka huu, ambapo taifa letu  lilipatwa na simanzi, pale wanafunzi 33 na walimu wao wawili pamoja dereva walipata ajali na kufariki papo hapo katika wilaya ya  Karatu, Mkoani Arusha. Kama sehemu mojawapo ya Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani, Mtandao wa wadau kutoka Asasi za Kiraia unaotetea Marekebisho ya Sheria na Sera inayohusu Usalama Barabarani Tanzaniasiku ya tarehe 12 na 13 Mei, 2017 wamefanikiwa kukaa na baadhi ya Wabunge kutoka kamati saba za Bunge. Kamati hizo ni Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Katiba na Sheria, Kamati ya Bajeti, Huduma za Jamii,  Kamati ya Sheria Ndogo, Viwanda na Biashara pamoja na Kamati ya Miundombinu. Vikao na Kamati hizo viliongozwa chini ya Uenyekiti wa Mwenyeketi wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajabu ambaye pia ni Mbunge wa Muheza. Katika Vikao hivyo Wabunge  walionyesha dhamira kubwa na kuunga mkono mapendekezo ya kuboresha usalama bararani kwa maendeleo ya Taifa letu. Wajumbe wa Kamati hizi walipata nafasi ya kusikiliza mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya usalama barabarani. Kwa mujibu wa moja ya mada hizo iliyyoelezea hali ilivyo sasa, ilielezwa kuwa madhara yatokanayo na ajali za barabarani yamemeendelea kuwa sababu namba tisa katika kusababisha vifo vya watu wengi zaidi duniani. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 1.25 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani. Wakati huo huo, watu zaidi ya milioni 20 hadi 50 wamebaki na majeraha makubwa na au ulemavu wa kudumu kutokana na ajali hizo kwa mwaka. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2015. Kwa mujibu ya ripoti ya haki za binadamu kwa mwaka 2016, ajali za barabarani zilipungua katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016, ikilinganishwa na kipindi kama hicho hicho kwa mwaka 2015. Jumla ya ajali 5,152 ziliripotiwa kwa Jeshi la Polisi kuanzia Januari hadi Juni 2016. Pia takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka watu 3,000 hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani Nchini. Aidha kwa upande wa Tanzania Bara, taarifa kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha  Usalama Barabarani inaonyesha kwamba, kwa mwaka 2016  jumla ya watu 3,256 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.  Katika vifo hivyo  wanaume ni 2,580 na wanawake ni 676.  Aidha kumekuwa na majeruhi 8,958 kati  yao wanaume ni 6,470 na wanawake 2,488. Wakati vyombo vya moto vilivyoongoza katika ajali ni magari binafsi ambayo yalisababisha ajali 3,649 ikifuatiwa na pikipiki zilizosababisha ajali 2,544 Kutokana na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini, Mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera zinazohusu usalama barabarani Tanzania  umeona  umuhimu na kuchukulia jambo hili na kulifanyia kazi kwa kina. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 76 ya ajali zote zinatokana na vyanzo vya kibinadamu kama vile Ulevi, Mwendokasi, Uzembe, Uchovu, kupuuzia au kutokuwa makini uwapo barabarani na kutokutii sheria za Usalama Barabarani. Tuna amini matendo haya ya kibinaadamu yanadhibitika kisheria, hivyo basi tunaisihi serikali kuboresha sheria. Kama wadau wa Usalama Barabarani, tunadhani kuna umuhimu wa sheria sasa kuboreshwa, na hivyo utashi wa kisiasa unatakiwa.  Ndiyo maana tukaitisha majadiliano ya pamoja na Wabunge pamoja na wadau mbalimbali wa Usalama Barabarani ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuleta mabadiliko ya sheria kwa ufanisi na kwa haraka.  Umoja wa mataifa na Shirika la Afya Duniani wanakiri kwamba sheria  madhubuti zinahitajika katika kupunguza idadi ya watu wanaofariki katika barabara zetu. Tanzania lazima tuwe na sheria kali za usalama barabarani kukomesha hali hii. Katika muda wa miaka mitatu iliyopita Nchi karibia 17 zinazowakilisha wananchi milioni 409 zimetunga na kufanyia maboresho ya sheria angalau kwa kiashiria kimoja au zaidi ambavyo vimekuwa ndio vyanzo vikubwa vya ajali na Nchi hizo zimekuwa zikifanya vizuri katika kudhibiti ajali. TanZania si miongoni mwa nchi hizo. Ni muda mwafaka sasa Tanzania kuchua hatua kwa matendo. Wabunge waliohudhuria vikao hivi kwa ujumla wao waliona umuhimu wa kuwa na mikakati ya kitaifa ya kupunguza ajali na walionyesha nia na kukubali kuunda Mtandao wa Wabunge wanaotetea usalama barabarani. Maeneo ambayo tunayapa kipaumbele katika maboresho ya sheria ni kama haya yafuatayo: a)     Matumizi ya mikanda; Sheria ya sasa ya Usalama barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria hiyo hiyo haisemi chochote kwa abiria wanaokaa kiti cha nyuma. Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unasema kuwa iwapo ajali ikitokea madhara/athari kwa abiria wa kiti cha mbele itapungua kwa 50% na kwa abiria wa nyuma madhara yatapungua kwa 70%. Kanuni zilizotungwa na SUMATRA zinataka abiria wote wafunge mkanda ila kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hili utekelezaji wa kanuni unakuwa mgumu. Hivyo basi ni rai yetu sheria hiyo ibadilishwe na kuwataka abiria wote wanaokuwa katika chombo cha usafiri wa kibiashara au binafsi kufunga mkanda wakati wote wa safari. b)    Matumizi sahihi ya kofia ngumu; Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa ni kosa kwa muendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu wakati wa kuendesha chombo hicho. Lakini sheria hiyohiyo haisemi chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho.  Vilevile pamoja na kuanisha kosa kwa dereva wa pikipiki kutokuvaa kofia ngumu lakini pia sheria haielezi ni jinsi gani kofia inatakiwa kuvaliwa na aina maalum ya kofia inayotakiwa kuvaliwa. Kwa mujibu wa Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO)  unaonyesha kuwa iwapo ajali itatokea madhara yanayotokea kwa kutovaa kofia maalum na kwa usahihi ni makubwa sana ukilinganisha na kofia hiyo ikivaliwa  kwa usahihi. Hivyo basi ukizingatia kuwa sasa hivi usafiri wa pikipiki umekuwa unatumika kwa kiasi kikubwa (public transport) hivyo ni rai yetu sheria hiyo ifanyiwe maboresho na kuweka kuwa ni sheria kwa mtu yoyote anayepanda pikipiki kuvaa kofia ngumu na kwa usahihi. c)     Ulevi: Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika mfumo wa mwili. Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani na kupendekeza kiwango cha asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea (experienced driver) na asilimia 0.02% kwa dereva  mchanga (young driver). Hivyo basi ni rai yetu kuwa sheria ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti. d)    Mwendo kasi (Speeding): Mwendokasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi. Sheria yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la Polisi na wadau wengine kutaka kudhibiti jambo hili limeendelea kuwa tatizo. Adhabu zisizokidhi wala kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii zimeendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo hili.  Tunatoa wito kwa watunga sera kushirikiana zaidi na wadau kuuelimisha umma katika eneo la uhusiano wa adhabu zitokanazo na makosa ya usalama barabarani na ongezeko la ajali. Pia sheria kufanyiwa maboresho na kuangalia kwa upya mianya iliyopo. TAMKO HILI LIMETOLEWA LEO NA MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA: TAWLA TAMWA WLAC TCRF TLS TMF RSA AMEND TANZANIA SHIVYAWATA TABOA & SAFE SPEED FOUNDATION  

Viewing all articles
Browse latest Browse all 40

Trending Articles