Chama cha Wanahabari Wanawake nchini- TAMWA kinalaani vikali ucheleweshwaji na upotoshwaji ushahidi wa kesi za vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa za ubakaji na ulawiti katika ngazi ya mahakama, polisi na baadhi ya madaktari hospitalini.
Hali hiyo imekuja baada ya TAMWA kubaini kuwa kesi 62 za ubakaji zimeshindwa kutolewa hukumu/ uamuzi na mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka 2014-2015
Kati ya kesi 63 za ubakaji, ni kesi moja tu mtuhumiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi 43 bado ziko mahakamani, kesi 17 zimeshindwa kufika mahakamani, ambapo kesi mbili zimefutwa kwa kukosekana ushahidi.
Mahakama zinazolalamikiwa ni pamoja na ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Ilala na Temeke, na kwa upande wa hospitali baadhi ya madaktari wamekuwa wakiwaomba walalamikaji (waathirika) pesa ili fomu zao zinazojulikana kama form namba 3
(PF3) zijazwe ukweli vinginevyo zijazwe uongo. Sambamba na hilo, madaktari wengine wamelalamikiwa kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ama ndugu na jamaa za watuhumiwa ili fomu hizo zijazwe kwa kupotosha ukweli.
TAMWA inalaani vitendo vya baadhi ya madaktari kujaza fomu za PF3 umri wa uongo na majina ya walalamikaji ambayo si ya kweli. Kwa mfano kesi ya ubakaji kwa mtoto wa miaka 9, fomu yake ilipotoshwa ikaandikwa kuwa mtoto aliyebakwa alikuwa na umri wa miaka 19, ikaambatanishwa kwenye jalada lililokwenda kwa mwanasheria wa serikali, kesi hiyo haikupelekwa mahakamani kwani illikosa ushahidi.
Aidha TAMWA inaesikitishwa na vitendo vya baadhi ya polisi kuwaambia wazazi wa watoto waliofanyiwa ukatili wa ubakaji ama ulawiti kuwa wakayamalize na mtuhumiwa nyumbani. Sambamba na hilo baadhi ya polisi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwa mlalamikaji ambapo wanatoa maneno ya vitisho na kupelekea mlalamikaji kukosa ujasiri wa kuhifadhi na kutetea kesi yake na wakati mwingine mama mzazi anaandikwa kama mlalamikaji wa ubakaji badala ya mtoto mwenyewe ambaye ndiye mhanga wa ukatili huo.
TAMWA inaunga mkono tamko la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Joseph Pombe Magufuli alilotoa Siku ya Sheria Duniani tarehe 04/02/2016 linalosema, kila hakimu wa mahakama anapaswa kuhukumu kesi si chini ya 260 kwa mwaka na kwa haki.
Aidha, TAMWA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali watetezi wa haki za binadamu katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ukeketaji, vipigo kwa wanawake, utelekezaji wa wanawake na watoto hapa nchini.
TAMWA inaamini kuwa juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia hasa ubakaji zinaweza kufanikiwa endapo tu, vyombo vya mahakama, dawati la jinsia, madaktari, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wakiwa mstari wa mbele kusaidia kuhakikisha kesi husika zinafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa wakati, kwa haki na kwa mujibu wa sheria.
Edda Sanga
Mkurugenzi Mtendaji