Quantcast
Channel: TAMWA - TAMWA - PRESS RELEASE
Viewing all articles
Browse latest Browse all 40

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KULAANI UKATILI DHIDI YA WANAWAKE UNAOKITHIRI NCHINI

$
0
0
Ndugu Wanahabari,  Taasisi zinazotetea haki za Wanawake na watoto nchini, tunalaani vikali ukatilii dhidi ya wanawake unaondelea kukithiri nchini.  Tukio la udhalilishaji wa Kijinsia kwa mwanamke mmoja lililotokea hivi karibuni katika mji mdogo wa Dakawa, wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, na kusambazwa kwa video ya udhalilishaji huo kwenye mitandao ya kijamii ni moja ya matukio ambayo hayapaswi kufumbiwa macho.  Huu ni udhalilishaji mkubwa na ukatili ambao amefanyiwa mwanamke huyu, na ni kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002) ambayo imeainisha makosa ya kujamiiana.  Pamoja na sheria za ndani, Serikali yetu imeridhia mikataba na matamko mengi kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia mfano mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW); pamoja na Mkataba wa haki za watoto (CRC), Tamko la Kimataifa la haki za binadamu (UDHR 19) ambalo linatambua haki za wanawake na watoto kama mojawapo ya haki za binadamu.
Taarifa tulizokusanya juu ya matukio ya Ukatili wa Kijinsia kwenye vyombo vya habari zinaonesha kwamba tukio hili la Morogoro, ni mwendelezo wa matukio mengine mengi ambayo yamekuwa yakiripotiwa kutokea sehemu mbalimbali nchini Tanzania, kwa mfano Mwezi Aprili mwaka huu, Yunis Peter mkazi wa jiji la Dar es Salaam ameuwawa kikatili kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni katika nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Sayari Guest House- mji mdogo wa Ifakara wilayani Kilombero, Rehema Lubinza (47) mkazi wa Tumaini wilayani Mlele, aliuawa kikatili kukatwa mapanga na mumewe kisha mwili wake kufungiwa ndani ya nyumba yake kwa siku tatu. Tukio jingine ni lile la Muuguzi wa zahanati ya Kagu Wilayani Geita Elizabeth Misango (54) ambaye aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana, gazeti la Mwananchi la tarehe 15/05/206 Uk. Wa 35 lilitolewa taarifa juu ya mwanamke aliyebakwa na Mganga wa Kienyeji. Vilevile tukio lililotokea huko Kaole kata ya Dunda wilayani Bagamoyo ambapo Flowin Peter Mbwale akiwa na rafiki yake Rajabu Juma (20) waliwaua Oliver Erasto (22) na mtoto Emanuel Flowin (3) kwa kuwachinja shingoni kwa kutumia kisu. Matukio haya na mengine yanaashiria kwamba kundi kubwa la wanawake linateketea kwa kushambuliwa kikatili; lakini pia matukio haya yanapelekea jamii kuona kwamba ni jambo la kawaida kumkandamiza mwanamke na kumtendea itakavyo kutokana na maumbile yake kibaiolojia na hii ni lazima serikali na vyombo vyake wachukue hatua za haraka. Ndugu Wanahabari,  Sisi taasisi tunaotetea haki na usawa wa kijinsia, tunavitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za haraka kuhakikisha watuhumiwa ambao wameshakamatwa kutokana na matukio haya ya Ukatili wa Kijinsia kesi zao ziendeshwe kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa ili haki itendeke na iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.  Tunautaka umma wa watanzania, kuendelea kusaidia vyombo vya dola ili vifanye kazi yake vizuri kwa kutoa taarifa za watuhumiwa wa Ukatili wa Kijinsia na kuwa tayari kutoa ushahidi pale wanapohitajika kufanya hivyo ili kukomesha kabisa matukio kama haya.  Tunaitaka jamii pia kuacha mashambulizi dhidi ya wanawake, na watoto yanayoendelea kuripotiwa nchini. Kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria na matamko mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia.  Tunawataka watanzania kuachana mara moja kusambaza video au picha za udhalilishaji wa wanawake, watoto, wazee au makundi yoyote ambazo zinaonesha faragha au kudhalilisha kwa namna yoyote kwani ni kinyume na sheria na Katiba ya nchi. Imetolewa leo Mei 18, 2016 na: Mashirika yafuatayo:   Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)   Kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake (WLAC)   Chama cha wanawake wanasheria Tanzania (TAWLA)   Kituo cha sheria na Haki za Binadamu (LHRC)   Women Fund Tanzania (WFT)

Viewing all articles
Browse latest Browse all 40

Trending Articles