Chama cha Wanahabari Wanawake TAMWA, kimeandaa mafunzo ya siku mbili yatakayofanyika kuanzia leo tarehe 13 na 14 Aprili, 2016 yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kamati zinazoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ili kuongeza uelewa wa kuvitolea taarifa vitendo hivyo.
Mafunzo hayo ya kamati na waadishi wa habari yatafanyika wilaya katika ya Mvomero mkoani Morogoro, wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, na wilaya Ruangwa mkoani Lindi zikiwa ni miongoni mwa wilaya 10 za Tanzania Bara na Visiwani, ambazo kwa kushirikiana na TAMWA zinatekeleza mradi wa Kujenga, Kuimarisha Usawa wa Kijinsia, na Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hapa nchini (GEWE II).
Tangu mwaka 2012, TAMWA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu hasa wanawake na watoto, kiliunda kamati za kushughulikia ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya vijiji hadi kata katika Wilaya 10 za Tanzania Bara na Visiwani.
Aidha, TAMWA katika utekelezaji wa mradi wa GEWE II kupitia Kamati za kushughulikia ukatili wa kijinsia, kwa kushirikiana na vyombo vya habari, watu wamekuwa wakivitolea taarifa vitendo hivyo, vikiandikwa na kutangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kutoka asilimia 56.9 kwa mwaka 2012 kabla ya kuanza kwa mradi mpaka asilimia 69.2 mwaka 2014 baada ya utekelezaji wa mradi.
Jumla ya watoa habari 120, wasaidizi wa sheria 120 na waragibishi 120, polisi, Viongozi wa dini, afya walipewa mafunzo jinsi ya kushughulikia ukatili wa kijinsia na wanaendelea na zoezi la kuratibu shughuli hizo katika ngazi za vijiji hadi kata.
GEWE II ni Mradi unaotekelezwa na TAMWA ambao ulianzishwa kwa lengo la kujenga, kuimarisha usawa wa kijinsia, na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini katika wilaya kumi za Tanzania bara na Visiwani zikiwemo Wete (Pemba Kasikazini), Unguja Mjini Magharibi (Unguja Magharibi), Unguja Kusini, Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Mvomero (Morogoro), Lindi vijijini na Ruangwa (Lindi), Kinondoni na Ilala Dar es Salaam
Edda Sanga
Mkurugenzi Mtendaji
↧